Tuesday, 29 January 2013

Gesi utata mtupu

Spika awafunga wabunge midomo.



SAKATA la ujenzi wa bomba la kusafirisha gesi asili kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, linaendelea kuwa utata mtupu kwa Serikali ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kutokana na usiri uliotanda mradi huo.
Rasilimali hiyo imezua vurugu kubwa mkoani Mtwara hivi karibuni na kusababisha vifo vya watu kadhaa pamoja na uharibifu wa mali za serikali na viongozi wa kisiasa, huku wananchi wakitaka waelezwe jinsi watakavyonufaika.
Hata hivyo, utata mkubwa umenza kujitokeza katika suala hilo kutokana na wawekezaji wa mradi huo kutishia kujitoa endapo mgogoro huo usipopatiwa ufumbuzi haraka.
Tanzania Daima Jumatano limedokezwa kuwa, kutokamilika kwa sera ya gesi ni sababu mojawapo inayochangia kukuza mgogoro huo kwani hadi sasa haijulikani nani ananufaika katika nini kama ilivyo kwenye mataifa jirani yenye sera za gesi.
Pia mgongano wa kimaslahi miongoni mwa vigogo wa CCM unatajwa kuwa chimbuko lingine la vurugu za Mtwara, kwani baadhi ya vigogo wa juu serikalini na kwenye chama wanadaiwa kuwa na uhusiano na makampuni yanayotaka kuchimba gesi hiyo.
Katika kile kinachoonekana kama mkakati wa serikali kufifisha hoja hiyo, tayari mizengwe imefanyika na kulishawishi Bunge lisiruhusu wabunge kujadili suala hilo.
Spika ayeyusha hoja
Spika wa Bunge, Anna Makinda ametangaza kuzikataa hoja binafsi zinazolenga kujadili sakata la gesi asilia mkoani Mtwara, jambo lililotafsiriwa kama njama ya kutaka kuwaziba midomo wabunge.
Makinda alitoa uamuzi huo wa kutojadili suala hilo bungeni kwa madai kuwa ni zito na nyeti, linalopaswa kujadiliwa kwa hekima kubwa na busara ya kutosha ili kupata muafaka wa kweli.
Aliliambia Bunge jana kuwa, kutokana na unyeti wake ataunda tume bila kubainisha itakuwa ya watu wangapi ambayo itazungumza na wananchi wa Mtwara pamoja na viongozi wa serikali na makundi mbalimbali na baadae itarejesha majibu bungeni na ndipo suala hilo litaweza kujadiliwa.
“Nimefikiria sana kuhusu suala la gesi, nimeona hakuna sababu yoyote ya kuwepo kwa hoja binafsi wala kuruhusu wabunge walijadili suala hilo hapa bungeni, bali busara ni kuundwa tume ambayo itafanya kazi ya kufuatilia suala hilo kwa makini na kupata majibu,” alisema.
Makinda aliongeza kuwa, tume hiyo itafanya kazi ya kuzungumza na wananchi pamoja na makundi mbalimbali mkoani Mtwara, wakiwemo pia viongozi wa serikali na baadae itarejesha majibu ambayo yatawasilishwa bungeni.
Alisema tume hiyo ni lazima ifanye kazi ya kuzungumza na kubaini tatizo ni nini ili liweze kupatiwa ufumbuzi badala ya kujadili jambo ambalo kiini chake hakijulikani sawa sawa.
Kwamba tume itahakikisha inaleta majibu mapema iwezekanavyo katika Bunge linaloendelea mjini hapa.
Mawaziri wakinzana
Wakati spika akizima hoja hiyo kiaina, Waziri wa Nishati na Madini, Prof. Sospeter Muhongo na Naibu wake, George Simbachawene wametofautiana kuhusu gharama halisi za ujenzi wa bomba la gesi asilia toka Mtwara hadi Dar es Salaam.
Prof. Muhongo alisema gharama halisi za ujenzi wa bomba hilo ni dola za Kimarekani bilioni 1.2 wakati naibu wake aliwaambia wahariri wa habari mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa gharama halisi za mradi huo ni dola milioni 875,715.
Simbachawene alikwenda mbali zaidi na kumtuhumu mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA) kuwa anapotosha mradi huo na kuchochea wananchi kutokana na kukosa uzalendo.
Hata hivyo, Zitto alikataa kubishana na naibu waziri huyo kwa sasa akidai hawezi kufanya hivyo wakati nchi inaungua, na hivyo kuhoji usiri katika mkataba huo ni wa nini kama si kwamba serikali inaashiria kuficha kitu.
Katika mazungumzo yake na Tanzania Daima Jumatano, kwa njia ya simu jana, Waziri Muhongo alifafanua utata huo akisema haiwezekani naibu wake akatoa taarifa kama hiyo wakati tayari walishasema gharama halisi.
“Hata ukienda kwenye kumbukumbu za Bunge, hiyo ndiyo gharama halisi na tulishaomba mkopo kutoka Benki ya Exim ya China, hivyo naibu wangu hawezi kusema takwimu hizo unazonitajia,” alisema.
Kuhusu utekelezaji wa mradi wa mpango kabambe wa umeme nchini (Power System Master Plan) wa kujenga kituo cha kufua umeme 300MW Mnazi Bay, Mtwara na kujenga msongo wa umeme wa 300KV hadi Singida ambao Rais Jakaya Kikwete alipokea ripoti ya ujenzi wake Oktoba 12, 2011, Muhongo alisema hawezi kuuzungumzia.
“Sasa ni mwaka 2013, siwezi kuzungumzia vitu vya mwaka 2011, kuna mabadiliko mengi yameshafanyika,” alisema.
Rais Kikwete alipokea ripoti ya ujenzi wa mradi huu kutoka makampuni ya China National Machinery & Equipment Import & Export Corporation (CMEC) ya China na Siemens ya Ujerumani, ambayo kwa pamoja yalitarajia kujenga kituo kikubwa cha kuzalisha umeme kutokana na gesi katika eneo la Mnazi Bay, mjini Mtwara.
Mradi huo ungehusisha kujenga njia ya kusafirisha umeme ya kilomita 1,100 kutoka Mtwara hadi Singida na ungegharimu dola za Kimarekani milioni 684 na Rais aliagiza utekelezwe haraka sana.
Ni katika utata huo Zitto alimtaka Waziri Muhongo afafanue mradi huo uliishia wapi na kwanini serikali ipo kimya kuhusu mradi huu ambao ungejibu kabisa maswali ya watu wa Mtwara.
CHADEMA yambana Kinana
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema kuwa kauli za Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye za kuitaka serikali ikae na wananchi wa Mtwara sasa ni za kinafiki.
Hatua hiyo inakuja siku moja baada ya viongozi hao kunukuliwa na vyombo vya habari wakiitaka serikali ikae na wananchi wa Mtwara na kusikiliza madai yao katika sauala zima la gesi asilia.
Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika alisema unafiki wa kauli za Kinana na Nape unatokana na kukinzana na kauli za viongozi wenzao wa juu, yaani mwenyekiti wao, Rais Jakaya Kikwete na Makamu wake - Bara, Philip Mangula.
Mnyika alisema Rais Kikwete alinukuliwa na vyombo vya habari akipuuza madai ya watu wa Mtwara na kuwaita wachochezi walipoandamana kuhoji rasilimali yao.
“Kauli za kujikosha za Kinana na Nape haziwezi kurudisha nyuma vuguvugu la wananchi kufanya mabadiliko kwa kuiondoa CCM madarakani kupitia chaguzi za mwaka 2014 na 2015 na kuiunga mkono CHADEMA katika mpango mkakati wake wa mwaka 2013,” alisema.
Mnyika ambaye pia ni mbunge wa Ubungo, alisema kuwa CHADEMA imekuwa mstari wa mbele kupambana na ufisadi na kutetea rasilimali za taifa pamoja na kuwa na sera sahihi zenye kuwezesha maendeleo endelevu ya wananchi.
Alisema kwa kuzingatia misingi hiyo, kikao cha Baraza Kuu la dharura cha CHADEMA kiliazimia msimamo wa Kamati Kuu kuhusu mgogoro wa gesi Mtwara kwamba wanataka wananchi wasikilizwe na serikali isimamishe mchakato wa kuvuna gesi yao hadi itakapokuwa imetekeleza mambo kadhaa.
Mnyika alitaja mambo hayo kuwa ni kuweka wazi mikataba yote ya utafutaji na uvunaji wa gesi ili wananchi wajue inalinda maslahi yao na si kuwanufaisha viongozi wa CCM.
“Kwanini serikali haitaki kujenga vinu vya kufua umeme kwa kutumia gesi pale Mnazi Bay Mtwara, na kuingiza umeme wa 300 MW katika gridi ya taifa?
“CCM ijieleze kwa kushindwa kutekeleza ilani yake kuhusu ahadi hii, iseme kwanini haiwezi kujenga mitambo ya kufua gesi Mtwara, na badala yake inang’ang’ania kujenga mabomba ya kupeleka gesi Bagamoyo na Dar es Salaam,” alisisitiza.
Mnyika alisema Kinana ni lazima atoe kauli kama aliyoitoa juzi kwani alikuwa ni sehemu ya uongozi wa bodi ya wakurugenzi ya Kampuni ya Artumas na alishiriki kuwakosesha wananchi wa Mtwara fursa ya umeme wa MW 300 zilizopaswa kuzalishwa Mnazi Bay tangu 2009.
“Kinana badala ya kujifanya kuwatetea wananchi wa Mtwara awaeleze alilipwa kiasi gani na kampuni hiyo na kwanini hakutetea maslahi ya wananchi toka wakati huo,” alisema.

0 comments:

Post a Comment